Sunday 14 February 2010



SIKU ya wapendanao huadhimishwa kila ifikapo tarehe 14 Februari ya kila mwaka.
Watu wengi wanaosherekea siku hii kwa Nchi za Afrika Mashariki ni vijana walio kati ya miaka 18 hadi 35.
Historia ya sikukuu hii inaanzia miaka mingi jijini, Roma, Italia ikiwa inahusishwa na mtakatifu Valentine au Valentinus aliyekuwa akiishi jijini humo katika karne hiyo.
Wakati wa maisha ya mtakatifu Valentine Roma ilikuwa ikitawaliwa na Kaisari, Claudius II, ambaye alipata hisia wakati huo kuwa askari mkakamavu na bora zaidi ni yule asiyekuwa na mke wala familia (kapera).
Claudius alilifanyia kazi wazo lake na aliamua kupiga marufuku ndoa zote kwa askari wa nchi hiyo, jambo ambalo halikukubaliwa na mtakatifu, Valentinus.
Hivyo Valentinus alichukua jukumu la kukaidi amri ile na kuendelea kuwafungisha ndoa kwa siri maaskari waliokuwa wakitaka kufungishwa ndoa.
Haikuchukua muda mrefu, taarifa zilimfikia mfalme, Claudius na alipopata habari hizo aliamuru kukamatwa na kufungwa gerezani na kisha Valentinus aliuawa kwa amri ya Kaisari.
Kuna taarifa zinadai kuwa kabla ya kuuawa kwa Valentine wakati huo akiwa amefungwa, mtakatifu Valentine aliandika barua ya salamu kwa binti aliyekuwa amekwenda kumsalimia gerezani.
Na mwisho wa barua kulisomeka maneno yaliyoandikwa ‘From your Valentine.’
Tangu hapo Valentine akawa anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na siku hii ikawa inaadhimishwa duniani kote.
Baada ya kufariki kwa mtakatifu huyo ndipo wananchi wengi duniani wakaamua kuadhimisha siku hii kama sherehe ya kumkumbuka Mtakatifu Valentinus.
Namna sherehe hii inavyosherehekewa hivi sasa
Katika nyakati zetu hizi siku ya wapendanao au siku ya mtakatifu Valentine inayosherehekewa Februari 14 ya kila mwaka na watu wengi duniani, wakazi wa Nchi za Magharibi husherehekea siku hii kwa kutumiana kadi zenye maandishi ya Valentine, maua mekundu yanayoonyesha ishara ya mapendo.
Watu wengi wamekuwa wakiisherehekea kwa kula pamoja ikiwa ni pamoja na kutumiana kadi.
Mapambo ambayo yamekuwa yakitumika katika sherehe hizi ni yale yaliyotengenezwa katika umbo la moyo ikimaanisha mapendo ya kweli.
Maendeleo ya kutumiana kadi yalianza tangu karne ya 18, ikawa kama mtindo ulioonekana kupata umaarufu zaidi hadi ilipofikia karne ya 19 katika nchi za Uingereza.
Katika nchi ya Marekani na Amerika ya Kusini mtindo huu wa kutumiana kadi ulishika umaarufu kwenye karne ya 19 wakati huo ikifanywa kama moja ya sherehe kubwa nchini humo.
Wakati ukiingia Marekani wafanyabiashara wakubwa wa kadi katika nchi hiyo walifanikiwa kuuza zaidi ya kadi bilioni moja ndani na nje ya nchi hiyo, idadi iliyoikaribia ya uuzaji wa kadi za Siku kuu ya Krismasi.
Wengi wa watu ambao wamekuwa wakionekana kuisherehekea siku hii wamekuwa wakifikiria kuwa ni siku ambayo maalum ya uzinifu na kufanya uasherati, kumbe sivyo.
Nchi ya China, wananchi wake husherehekea siku hii kwa kupeana zawadi ya chokoleti, maua kwa wanawake ambao wanawapenda na wamekuwa wakiita kwa jina la pinyin.
Japan sikukuu hii inajulikana kama Tanabata, ambako wao huisherehekea Julai 7 kila mwaka.
Kwa upande wa nchi ya Saudi Arabia mwaka 2008, walichukua jukumu la kuchoma kadi zote za Valentine katika maduka yaliyoziingiza katika nchi hiyo, wakiwa wanashutumu kuwa siku hiyo ni maalumu kwa ajili ya Wakristo na si kwa Waislam.

No comments:

Post a Comment